Jinsi ya kuwatumia wasomaji habari unazoandika

April 16, 2006

Yapo mambo kadhaa ambayo mwenye blogu anaweza kufanya ili kusaidia wasomaji kwa kurahisisha upatikanaji wa habari unazoandika. Kati ya mambo hayo ni huduma inayowezesha wasomaji kutumiwa mambo unayoandika kwa barua pepe. Msomaji anachotakiwa kufanya ni kuweka anuani yake kwenye fomu utakayoweka kwenye blogu yako kisha atatumiwa habari mpya kila unapoandika. Huduma nitakazokupa ni za bure (ingawa zipo pia za kulipia). Kama ungependa kuwapa wasomaji wako huduma hii, unaweza kutumia huduma kati ya hizi nitakazoorodhesha hapo chini. Ukiwa na tatizo ya jinsi ya kutumia huduma hizo au kuziweka kwenye blogu yako unaweza kuniandikia: ughaibuni@yahoo.com (HAKIKISHA KICHWA CHA WARAKA WAKO KINASEMA: MWONGOZO WA BLOGU)(LA SIVYO BARUA YAKO INAWEZA IKACHUKUA MUDA MREFU KUSOMWA).

Huduma ni hizi:

1. FEEDBLITZ: http://www.feedblitz.com/

2. SQUEET: http://www.squeet.com/

3. YUTTER: http://www.yutter.com/

4. AWEBER: http://www.buniek.com/

5. ZOOKODA: http://www.zookoda.com/

Advertisements

Huduma za kuhifadhi makala ndefu na Jinsi ya kuweka makala bloguni

April 15, 2006

Iwapo unaandika makala ndefu (waandishi wa habari hupenda kuita makala ndefu “mikeka”) au labda wewe ni mwanasafu na unapenda kuweka makala zako kwenye blogu yako, zipo huduma kadhaa ambazo unaweza kutumia ili kuhifadhi makala hizo. Kisha utanakili anuani ya makala zako toka kwenye huduma uliyotumia na kubandika kwenye blogu yako. Msomaji akibonyeza ulipoweka kiungo cha makala hiyo ataweza kuisoma. Huduma hizi ni za bure (zipo pia za kulipia ila nadhani hakuna sababu za msingi za kuacha kutumia huduma hizi za bure).

Huduma zenyewe:

1. Ripway: http://www.ripway.com

Huduma hii inatumiwa na wanablogu wengi wa Kiswahili. Huduma hii ni nzuri ingawa ina kiwango cha ukubwa wa mafaili ambayo unaweza ukahifadhi hapo. Unaweza kuhifadhi makala zenye ukubwa wa 30MB (jumla ya makala zote). Utahitaji kuwa na makala nyingi na ndefu sana kuweza kufikia kiwango hicho kwa haraka. Ukifikia kuwa na makala za ukubwa huo unaweza kuanzisha akaunti mpya kwa jina jingine! Pia kuna kiwango cha ukubwa wa mafaili ambayo yanaweza kusomwa katika kipindi cha masaa 24 ambayo ni 15MB. Wasomaji wakisoma makala zenye ukubwa zaidi ya huo akaunti yako itasimama kwa muda (baadaye itaendelea kufanya kazi).

Muhimu: usipoitumia akaunti yako katika kipindi cha mwezi mzima itafungiwa kwa muda. Hivyo lazima uwe unaingia ndani ya akaunti hiyo (hata kama huna makala mpya za kuweka) mara kwa mara.

2. Box: http://www.box.net/

Huduma ya Box inakuwa nafasi kubwa zaidi ya Ripway ya kuhifadhi makala au hadithi zako. Una nafasi ya ukubwa gigabaiti 1 (IGB) bure. Ukitaka nafasi zaidi itabidi ulipie. Huduma hii inakuwezesha kubandika kiungo cha makala au hadithi yako kwenye blogu yako kwa ajili ya wasomaji wako.

3. Freefilehosting: http://www.freefilehosting.org/

Freefilehosting wanakupa nafasi ya ukubwa wa 50MB na pia kiungo cha makala ulizohifadhi ili uweze kuweka kwenye blogu yako.

4. Gimehost: http://www.gimehost.com/

Huduma ya Gimehost, ingawa haijajengwa vizuri kama Ripway inaweza kuchukua makala zako utakazoandika maisha yako yote, Yaani hakuna ukubwa wa mafaili ambao ndio kikomo. Pia wasomaji wanaweza kusoma makala zako bila kuzuiwa pale watakapokuwa wamesoma makala za ukubwa fulani. Huduma hii inakupa kiungo ambacho utakiweka kwenye blogu yako.

Jinsi ya kuweka kiungo cha makala kwenye blogu yako:

Ukishachagua huduma unayotaka, ukapandisha makala, utapewa kiungo/anuani ya webu. Nakili kiungo/anuani hiyo kisha ingia ndani ya blogu yako.

Kama unataka kuwa na kona maalum ya makala zako kwenye ufito wa pembeni (sidebar) itabidi ujue jinsi ya kuweka kichwa cha habari cha kona za makala zako. Maelezo hayo hapo chini:

<h2 class=”sidebar-title”> HAPA WEKA KICHWA/JINA LA KONA YA MAKALA ZAKO</h2>

* Weka jina la makala yako katikati ya alama: > na < (kama ilivyo hapo juu).

Halafu jinsi ya kuweka makala zenyewe kwenye ufito wa pembeni (sidebar), yaani chini ya jina la kona yako ya makala. Utachukua anuani/kiungo ulichopata toka kwenye huduma ya kuhifadhi makala (nilizozielezea hapo juu) na kuweka katikati ya alama za kufungua na kufunga usemi kama ilivyo hapo chini:

<ul>

<li><a href=”HAPA UTAWEKA ANUANI/KIUNGO CHA MAKALA YAKO”>HAPA UTAWEKA KICHWA CHA MAKALA YAKO AMBACHO NDIO KITAONEKANA KWA WASOMAJI KWENYE BLOGU</a></li>

</ul>

Kwahiyo kila utakapokuwa unaweka makala itabidi utumie muundo huo hapo juu. Jambo la kuhakikisha ni kuwa makala zote lazima ziwe katikati ya alama <ul> na </ul>. Hizi ndio “code” za kufunga na kufungua kwahiyo mambo yote weka hapo katikati.

Mahali pa kuweka ndani ya blogu: itabidi uingie ndani ya blogu kwa kutumia neno lako la siri. Kisha nenda panaposema: “change setting”, halafu bonyeza kwenye “template.” Kisha ndani ya templeti tafuta sehemu ambayo utapenda kuweka kona ya makala zako. Templeti zinatofautiana na kila mtu ana upenzi wake wa eneo analotaka kuweka makala. Ila ni vyema ukaweka chini ya “code” zinazoweka kisehemu cha maelezo binafsi (profile). Popote chini ya hapo ni sawa.

Ukiwa na swali usisite kuniuliza: ughaibuni@yahoo.com au kumuuliza mwanablogu mwingine yeyote aliyebobea.

Jinsi ya kuanza kublogu

April 7, 2006

Iwapo huna blogu na unataka kuanza, huduma ambayo inaweza kuwa rahisi sana kwako ni huduma ya Blogger. Huduma hii ni ya bure na ndio huduma maarufu sana kwa wanablogu wa Tanzania. Hatua za kufuata ni chache sana na rahisi kueleweka. Huduma yenyewe ya Blogger, ambayo mimi nilikuwa naitumia hapo awali, pengine ndio rahisi zaidi ya huduma nyingine kwa mtu ambaye ndio anaanza kublogu. Kumbuka kuwa ukianza kublogu kwa kutumia huduma moja, ukafika wakati ukataka kutumia huduma nyingine, unaweza kuhamisha blogu yako hiyo toka huduma ya zamani kwenda huduma mpya. Mimi, kwa mfano, nilikuwa natumia huduma ya blogger. Lakini sasa natumia huduma ya WordPress. Nimeweza kuhamisha blogu yangu nzima nzima bila matatizo.

Kwahiyo kitu cha kwanza cha kufanya ni kwenda kwenye tovuti ya Blogger kwa kubonyeza hapa. Ukifika pale kwenye tovuti yao, tazama upande wa chini kulia kuna alama ya mshale wa rangi ya machungwa unaosema: Create your blog now. Bonyeza juu ya mshale hu. Utapelekwa hatua kwa hatua toka mwanzo hadi mwisho ambapo kwa dakika chache tu utakuwa na blogu yako mwenyewe.

Ukiwa una mambo unayohitaji msaada, tazama ndani ya blogu hii (upande wa kulia kwenye "categories") ambapo utaona maelezo ya jinsi ya kuweka picha, viungo, jinsi ya kutangaza blogu yako, n.k. Au niandikie, au mwandikie mwanablogu yeyote wa Kiswahili maana tuna utamaduni wa kusaidiana kama ndugu. Usidhani kuwa utakuwa unatusumbua. Tunablogu na tunapenda nawe ujiunge na kijiji chetu uanze kublogu. Karibu!

Jinsi ya kublogu kwa simu za mkono

April 7, 2006

Badala ya kublogu kwa kutumia tarakilishi (kompyuta) unaweza kublogu kwa kutumia simu ya mkono. Zipo huduma kadhaa, za bure na pia za kulipia, ambazo zinakuwezesha kutumia simu ya mkono kublogu. Huduma maarufu ya kublogu ya Blogger inayo huduma ya kublogu kwa simu (Audioblogger). Bonyeza hapa upate maelezo ya jinsi ya kutumia huduma hiyo. Kumbuka: lazima ujiandikishe kwanza kwenye huduma ya Blogger ili uweze kutumia huduma ya Audioblogger. Jinsi ya kujiandikisha kwenye Blogger, bonyeza hapa.

Huduma nyingine ni Phoneblogz. Huduma hii inakuwezesha kutuma ujumbe wa sauti, kwa kutumia simu, kwenye blogu yako. Bonyeza hapa uione huduma hiyo. Kuna huduma iitwayo Gabcast. Huduma hii nayo inakuwezesha kutuma ujumbe wa sauti kwenye blogu yako. Lakini pia unaweza kuanzisha blogu ya sauti kwa kutumia huduma yao. Gabcast wana huduma ya bure na nyingine ya kulipia. Bonyeza hapa uende kwenye tovuti yao.

Huduma nyingine iitwayo Phlogger inakuwezesha kublogu kwa kutumia simu ya mkono ila badala ya kutuma ujumbe kwa sauti kama huduma nilizotaja hapo juu, huduma hii inakuwezesha kutuma ujumbe wa maandishi. Bonyeza hapa uitazame.

Kati ya Blogger na WordPress ipi bora?

February 19, 2006

Baadhi ya wasomaji kwenye blogu yangu wametaka kujua zaidi kuhusu huduma za kublogu za Blogger na WordPress. Nimelinganisha huduma hizo katika makala ambayo utaisoma kwa kubonyeza hapa kwanza kisha bonyeza hapa.

Jinsi ya kufupisha anuani ndeeeefu

February 15, 2006

Viungo virefu mara kwa mara huwa na matatizo. Kuna wakati vinakatika hivyo kutofunguka. Wakati mwingine ukivibandika kwenye ukurasa wa habari unayoandika vinakuwa virefu sana kupita ukubwa wa eneo la kuandikia habari yako. Ipo huduma ya kufupisha anuani ndefu za tovuti. Huduma hiyo iitwayo Tiny URL utaipata kwa kubonyeza hapa. Ukifika kwenye tovuti hiyo unachofanya ni kuweka anuani yako ndefu (baada ya kuinakili kwa kutumia “file” kisha “copy” au kwa kwa kuweka wingu juu ya anuani unayoitaka kisha kubonyeza Ctrl na C kwa wakati mmoja. Ukifika kwenye tovuti ya Tiny URL, bandika anuani hiyo panaposema “make long URL tiny.” Unaweza kufanya hivyo kwa kubonyeza Ctrl na V au kwa kutumia kipanya chako. Ukishaweka kwenye kisanduku hicho na kubonyeza, utapewa anuani mpya fupi ambayo ndio utaitumia kwenye blogu yako. Anuani hiyo akibonyeza mtu atapelekwa kule kwenye ile anuani ndefu.

Kwa mfano, tazama anuani hii fupi kirefu chake ni nini: http://tinyurl.com/8ksov

Fanya hivyo kwa kuibandika sehemu ya anuani za tovuti kisha bonyeza “enter” uone anuani nzima ilivyo ndefu.

Jinsi ya kuhamia WordPress toka Blogger

February 15, 2006

Naandika mwongozo huu wa namna ya kuhama toka Blogger (http://blogger.com  au http://blogspot.com) kwenda WordPress (http://wordpress.com) maana wanablogu wengi wa Kiswahili hivi sasa wanatumia huduma za Blogger.

WordPress ni huduma ambayo imetengenezwa kwa mtindo wa programu huria.  Hii inamaanisha kuwa wanaojenga programu hii na kuiboresha ni watu waliotapakaa pembe nne za dunia ambao wanafanya kazi hii kijamaa.  Zaidi ya kuwa kibinafsi ninapenda programu huria kutokana na itikadi na falsafa zangu binafsi, WordPress inatupa wanablogu uwezo wa kufanya mambo kadhaa ambayo yamekuwa hayawezekani kupitia Blogger.  Zaidi ya hilo, toleo la Kiswahili la WordPress liko njiani.  Soma hapa.  Utakapoanza kutumia WordPress utaona mwenyewe tofauti kubwa iliyopo kati yake na Blogger.  Kwa mfano, mpangilio wao wahabari katika maudhui na kisanduku cha kutafuta habari ulizoandika vinasaidia wasomaji kuweza kupata habari zako kwa urahisi.  Kwa mfano, ukija kwenye blogu yangu mpya ukataka kutafuta habari nilizoandika kuhusu Nyerere, unakwenda kwenye kisanduku cha kusaka habari na kuandika, “Nyererere,” ukibonyeza utapata habari zote nilizowahi kuandika kuhusu Nyerere. Upangaji wa habari kimaudhui unafanya habari zisipotelee kwenye “nyaraka” au “kumbukumbu” bali ziwe zinapatikana kwa urahisi.  Ni rahisi pia kupata kiungo cha habari yoyote tofauti na kwenye Blogger. Ukitaka kupata kiungo cha habari unayosoma (labda unataka kuweka kiungo hicho kwenye habari unayoandika kwenye blogu yako), unabonyeza juu ya kichwa cha habari yenyewe.  Utapalekwa kwenye kiungo chake.  Utaona kuwa kutokana na kutokuwa na mfumo huu kwenye Blogger, mwanablogu anaweza kuwa anazungumzia habari niliyoandika badala ya kuweka kiungo cha habari yenyewe akaweka kiungo cha blogu nzima. Kwa mfano, kiungo hiki ni cha blogu nzima: http://jikomboe.com, wakati ambapo kiungo hiki kinakupeleka moja kwa moja kwenye habari: http://www.jikomboe.com/?p=1108

Ukianza kutumia WordPress utaona ubora wake.  Unaweza kuanzisha blogu ya majaribio ili kutazama ilivyo.  Ukishaanzisha utaona kuwa WordPress ina mfumo mzuri wa “trackback” na “ping” ambao ni aina ya mawasiliano kati ya blogu na blogu.  Mifumo hii miwili inakuwezesha kujua nani ameweka kiungo cha blogu yako au habari uliyoandika kwenye blogu yake.  Mawasiliano haya anatokea bila wewe kufanya chochote. Taarifa hizi zinaingia zenyewe kwenye kidirisha cha maoni.

Hapo chini nimeweka maelezo yatakayokusaidia kama utakata shauri la kuhamia WordPress.  Kumbuka kuwa wakati wa kuhamisha blogu yakomambo kadhaa yatabadilika.  Itabidi uweke viungo upya na pia itakuwa vigumu picha kuhamishika moja kwa moja.  Soma maelezo:

Nenda http://wordpress.com

Bonyeza panaposema: Get a WordPress Blog Now.

WordPress watakutumia nywila (neno la siri) utakalotumia kuingia kwenye blogu yako.  Ukishaingia ndani ya blogu yako, nenda kwenye kisehemu kilichoko juu ya ukurasa kinachoitwa “Users.” Bonyeza hapo ili ubadilishe nywila waliyokutumia na kuweka nywila unayoitaka (ambayo utaikumbuka).

Ukishabonyeza hapo panaposema “Users,” tazama upande wa chini kulia ambapo utakuta panaposema, “Update your password.” Ukishachagua nywila mpya, bonyeza chini kabisa pasemapo, “Update profile.”

Baada ya hapo kazi inayofuata ni kuhamisha blogu yako toka blogger hadi wordpress. Kazi hii ni rahisi sana.  Tazama pale juu pembeni ya “Users,” utakuta panaposema, “Import.” Bonyeza hapo.  Kisha andika jina na neno la siri unalotumia kuingia kwenye blogu yako ya blogspot.com.   Halafu bonyeza panaposema, “start.” Jina la blogu yako litajitokeza. Bonyeza juu ya jina la blogu yako.  Wordpress itahamisha kila kitu toka blogger hadi wordpress.  Subiri hadi utakapoona maneno “congratulations.”  Hapo tazama chini kabisa kisha bonyeza panaposema, “Reset this importer.” Utaulizwa kama unataka kufanya hivyo au la. Bonyeza panaposema ndio.

Ili uone matokeo ya kazi uliyofanya, tazama juu kabisa, pembeni mwa jina la blogu yako hii mpya utaona panasema, “view site.” Bonyeza hapo utapelekwa kwenye blogu yako mpya ikiwa nay ale uliyoandika ukiwa blogspot.com .

Kutakuwa na mabadiliko kadhaa: kwa mfano picha si rahisi zihamishwe, viuongo ulivyoweka itabidi uweke upya, n.k.

Jambo muhimu na la kukumbuka ni kuwa kuanzia sasa utakuwa unaweza kuhifadhia kazi zako kwenye makundi ya kimaudhui.  Makundi haya (jina lake kwenye wordpress ni “categories”) unaweza kuyaweka wakati unapoandika jambo.  Ukiwa kwenye ukurasa wa kuandika jambo, tazama upande wa kulia utaona kuna mlolongo wa vitu ambapo “categories” ni mojawapo. Bonyeza  hapo, patatokea kisanduku ambacho utaweza kuandika jina la maudhui ya jambo unalotaka kuandika. Inaweza kuwa: utamaduni, siasa, muziki, safari, soka, n.k. Wewe utaamua.

Njia nyingine ya kuweka maudhui ni kwenda kwenye kisehemu cha “manage” kisha bonyeza kwenye kisehemu cha “categories,” halafu weka maudhui kwenye kisanduku cha “Add new category.”

Kumbuka kila unapoandika jambo lazima uweke alama ya vema kuonyesha ni katika maudhui gani au kundi gani unataka habari hiyo iwe.  Kama utaweka maudhui wakati unaandika habari na sio kupitia “manage” kisha “categories” (maelezo yake yako hapo juu) basi hutakuwa na haja ya kuweka alama ya vema maana alama hiyo itajiweka yenyewe.

Jinsi ya kutangaza blogu yako

February 5, 2006

Baada ya kufungua blogu ni muhimu sana kutumia njia mbalimbali za kuitangaza ili ujumbe wako uweze kufikia watu wengi. Kati ya njia unazoweza kutumia ni kusajili blogu yako kwenye tovuti za Google na Yahoo! ili watu wanapotafuta habari mbalimbali kwenye mtandao wa tarakilishi waweze kupata blogu yako iwapo ina habari ambayo wanaitafuta. Kusajili google.com bonyeza hapa. Kusajili yahoo.com bonyeza hapa.

Kuna mradi unaoorodhesha blogu za Waafrika uitwao BlogAfrica. Sajili blogu yako kwa kubonyeza hapa.

Mradi wa Global Voices wa Kituo cha Intaneti na Jamii cha Berkman kina ukurasa wa “Wiki” wenye orodha ya blogu zilizopangwa ki-nchi. Kwakuwa ukurasa huo unatumia teknolojia ya “Wiki” mtu yeyote anaweza kuweka blogu katika orodha hiyo. Iwapo umeshindwa kufanya hivyo unaweza kuniandikia, nitaweka blogu yako. Orodha hii ninaitembelea mara kwa mara, kuongeza blogu mpya na kuisafisha iwapo mtu kaongeza blogu kimakosa. Bonyeza hapa uende kwenye ukurasa huo.

Ni muhimu sana pia kuweka viuongo vya blogu za wengine kwenye blogu yako. Sio lazima wawe wanablobu wa Kiswahili au toka Tanzania. Kawaida wanablogu unaoweka viuongo vyao kwenye blogu yako, nao huweka kiungo cha blogu yako kwenye blogu yako na hivyo kupanua wigo wa wasomaji wako. Njia hii ni muhimu sana maana inajenga mtandao na ushirikiano wa wanablogu.

Kuwa na tabia ya kutembelea blogu za wengine na pia kutoa maoni (kwa kutumia anuani ya jina unalotumia kuingia kwenye blogu yako). Baadhi ya watu wanaweza kujua kuwa una blogu kwa kuona anuani ya blogu yako kwenye maoni uliyotoa kwa wengine.

Weka anuani ya blogu yako kwenye anuani yako ya barua pepe. Huduma kama gmail, yahoo mail, n.k. zinakupa mtumiaji uwezo wa kuweka aina ya saini ambayo itatokea katika kila barua pepe unayotuma. Mwisho wa barua yako unapoandika jina lako, ni vyema basi kukawepo na anuani ya blogu yako. Pia kama una kadi za kazi (zimezoeleka kwa jina la business card), weka anuani ya blogu yako.

Iwapo wewe ni mwandishi wa habari, jaribu kumshawishi mhariri wako ili anuani ya blogu yako iwekwe mwisho mwa kila habari uliyoandika au safu yako.

Unaweza pia kuweka kidude cha “feedburner” katika barua zako. Kidude hiki kinaonyesha vichwa vya habari vya mambo uliyoandika katika blogu yako. Mtu akibonyeza juu ya hicho kidude anapelekwa kwenye blogu yako. Soma kuhusu kidude hicho kwa kubonyeza hapa.

Njia nyingine ni kutuma habari kwa watu wote ambao una anuani zao za barua pepe. Tuma barua moja kwa wote ukiwaeleza juu ya blogu yako na pia ukiwataka wawaeleze wengine. Ni vyema kufanya hivi baada ya kuwa umeweka mambo ya kutosha kwenye blogu yako. Usikaribishe watu iwapo umeandika sentensi mbili tu. Tafadhali usisite kuuliza swali lolote au kutaka msaada.

Jinsi ya kuweka picha binafsi

February 5, 2006

Baadhi ya wanablogu wanapenda kuweka picha zao binafsi kwenye blogu zao. Wengine hawapendi. Kama una mpango wa kuandika bila kutaka kujulikana kwa urahisi wewe ni nani, hutaweka picha yako. Lakini kutokweka picha hakutazuia wewe kujulikana iwapo itatokea umetumia blogu yako kinyume cha sheria za nchi. Mara nyingi wanablogu wanaotoka nchi zenye serikali zinazotia ndani au kuua wanaozikosoa ndio ambao hawapendi kuweka picha zao. Ila moja ya njia ya kujenga uaminifu na kuaminika ni kutojificha. Kama unayosema ni kweli, huna haja ya kujificha, hasa kama maisha yako hayako hatarini. Unaweza kutumia jina lako halisi bila kuweka picha yako. Nadhani jambo la kwanza muhimu ni matumizi ya jina lako halisi. Picha ni baadaye. Sehemu hii itakupa maelezo ya jinsi ya kupandisha picha yako. Ili kuweza kuweka picha yako, lazima usome kwanza maelezo ya jinsi ya kuweka picha kwenye habari unayoandika. Maelezo hayo utayapata kwa kubofya hapa.

Maelezo kamili yako hapa.

Jinsi ya kuweka picha

February 5, 2006

Inawezekana unaandika habari ambayo ungependa kuambatanisha picha.  Picha huwa zinaipa habari yoyote ile nguvu zaidi.  Kwa mfano, habari ndefu yenye maneno tupu ni rahisi sana kuchosha.  Ukiweza kuambatanisha picha, fanya hivyo.  Lakini napenda ukumbuke kuwa matumizi ya picha za watu wengine bila ruhusa yao ni kosa la jinai.  Utaweza kutumia picha ya mtu bila ruhusa yake iwapo mwenye picha ametoa ruhusa picha hiyo itumiwe bila kumuomba ruhusa moja kwa moja au kumlipa.  Kumbuka kuwa ni muhimu kusema picha hiyo imepigwa na nani au umeitoa wapi.  Picha zilizo chini ya mfumo mbadala wa hatimiliki wa Creative Commons unaweza kuzitumia bila kuomba ruhusa au kumlipa mwenye picha, lakini ni lazima useme hiyo picha kapiga nani.  Bonyeza hapa utaona mfano wa picha ambazo mtu yeyote anaweza kutumia.  Kama unaandika jambo kuhusu Tanzania, blogu ya Issa Michuzi ina picha nzuri sana za kihistoria na za karibuni.  Kumbuka lazima umpe heshima yake kwa kumtaja kuwa ndio mwenye picha. Blogu ya Michuzi ya picha iko hapa.

Sasa nenda kwenye maelezo ya jinsi ya kuweka picha kwenye blogu yako. Bonyeza hapa.