Archive for the ‘Zana muhimu kwa wanablogu’ Category

Snap: Huduma ya Kuweka Picha Kwenye Viungo

December 31, 2006

Iwapo unapenda wasomaji wako kuona picha ndogo ya tovuti au blogu ambayo umeweka kiungo chake kwenye habari unayoandika, unaweza kutumia huduma ya Snap. Huduma hii inawezesha wasomaji kuweza kuiona tovuti au blogu kabla ya kubonyeza na kuitembelea.

Nimeijaribu huduma hii kwenye blogu yangu ya Jikomboe na imefanya kazi bila matatizo yoyote. Unachotakiwa kufanya ni kufuata maelekezo yaliyoko hapa. Au kama wewe unatumia huduma ya Blogger unaweza kupata maelezo hapa na kwa watumiaji wa WordPress, maelekezo haya hapa.  

Advertisements

Zana ya kutengeneza Blogu au Tovuti Yako

December 26, 2006

Mwezi wa nane mwaka huu niliandika kuhusu huduma ya Wetpaint ambayo inakuwezesha kujenga blogu, wiki, au tovuti yako mwenyewe bila kuwa na haja ya kujua lugha ya kujenga tovuti (HTML au nyinginezo) na pia bila kutakiwa kushusha programu yoyote kwenye kompyuta yako. Huduma kama hizi ni muhimu sana kwa watu walioko katika nchi za Kusini ambapo wengi wanatumia kompyuta ambazo sio zao (kwenye migahawa) hivyo inakuwa vigumu kushusha programu kwenye kompyuta hizo. Pia inakuwa vigumu kutumia muda mrefu kwenye kompyuta kujifunza mambo kama ujenzi wa tovuti toka A hadi Z. Bonyeza hapa usome niliyoandika kuhusu Wetpaint na huduma nyingine.

Sasa kampuni ya incuBeta ina huduma inayofanana kiasi na Wetpaint ambayo inaitwa Synthasite. Huduma hii bado iko kwenye matengenezo ila unaweza kuwapa anuani yako ili wakutaarifu itakapokuwa tayari. Bonyeza hapa.

Scoopt: Huduma Poa Kwa Wanablogu wa Picha na Wapiga Picha

December 26, 2006

Iwapo wewe ni mwanablogu wa picha au mpiga picha na ungependa uwe unauza picha zako, kuna huduma inaitwa Scoopt. Huduma hii inachofanya ni kutafuta vyombo vya habari ambavyo vitanunua picha yako kisha mnagawa mapato nusu kwa nusu. Wewe asilimia 50 na wao 50. Mchezo umekwisha. Ila picha zenyewe lazima ziwe zinauzika na sio picha za familia yako, mbwa wako, majirani wako, n.k. Bonyeza hapa utembelee tovuti ya Scoopt. Ukitaka kujua aina ya picha ambazo wanazipenda, bonyeza hapa.

Iwapo unatumia huduma ya Flickr kuhifadhi picha zako, na ungependa jamaa wa Scoopt wazipate picha zako, unashauriwa kutumia neno “scoopt” kama neno la kuashiria maudhui ya picha yako (kwa kiingereza “tag”).

Zana ya kutengeneza blogu au tovuti yako

August 12, 2006

Kuna zana mpya ambayo itawafaa sana watu wenye nia ya kuwa na tovuti, blogu, au wiki zao wenyewe lakini hawana ujuzi wa utalaamu unaotumika kutengeneza tovuti, blogu, au wiki.  Zana hii inaitwa Wetpaint. Kwa dakika chache na bila ujuzi wowote zaidi ya ujuzi wa kutumia tarakilishi, unaweza kuwa na blogu au tovuti yako mwenyewe. Bonyeza hapa ujionee mwenyewe. Majuzi niliandika kuhusu zana hiyo na nyingine zinazofanana katika blogu yangu, bonyeza hapa na hapa ili usome niliyoandika.

Jinsi ya kuwatumia wasomaji habari unazoandika

April 16, 2006

Yapo mambo kadhaa ambayo mwenye blogu anaweza kufanya ili kusaidia wasomaji kwa kurahisisha upatikanaji wa habari unazoandika. Kati ya mambo hayo ni huduma inayowezesha wasomaji kutumiwa mambo unayoandika kwa barua pepe. Msomaji anachotakiwa kufanya ni kuweka anuani yake kwenye fomu utakayoweka kwenye blogu yako kisha atatumiwa habari mpya kila unapoandika. Huduma nitakazokupa ni za bure (ingawa zipo pia za kulipia). Kama ungependa kuwapa wasomaji wako huduma hii, unaweza kutumia huduma kati ya hizi nitakazoorodhesha hapo chini. Ukiwa na tatizo ya jinsi ya kutumia huduma hizo au kuziweka kwenye blogu yako unaweza kuniandikia: ughaibuni@yahoo.com (HAKIKISHA KICHWA CHA WARAKA WAKO KINASEMA: MWONGOZO WA BLOGU)(LA SIVYO BARUA YAKO INAWEZA IKACHUKUA MUDA MREFU KUSOMWA).

Huduma ni hizi:

1. FEEDBLITZ: http://www.feedblitz.com/

2. SQUEET: http://www.squeet.com/

3. YUTTER: http://www.yutter.com/

4. AWEBER: http://www.buniek.com/

5. ZOOKODA: http://www.zookoda.com/

Huduma za kuhifadhi makala ndefu na Jinsi ya kuweka makala bloguni

April 15, 2006

Iwapo unaandika makala ndefu (waandishi wa habari hupenda kuita makala ndefu “mikeka”) au labda wewe ni mwanasafu na unapenda kuweka makala zako kwenye blogu yako, zipo huduma kadhaa ambazo unaweza kutumia ili kuhifadhi makala hizo. Kisha utanakili anuani ya makala zako toka kwenye huduma uliyotumia na kubandika kwenye blogu yako. Msomaji akibonyeza ulipoweka kiungo cha makala hiyo ataweza kuisoma. Huduma hizi ni za bure (zipo pia za kulipia ila nadhani hakuna sababu za msingi za kuacha kutumia huduma hizi za bure).

Huduma zenyewe:

1. Ripway: http://www.ripway.com

Huduma hii inatumiwa na wanablogu wengi wa Kiswahili. Huduma hii ni nzuri ingawa ina kiwango cha ukubwa wa mafaili ambayo unaweza ukahifadhi hapo. Unaweza kuhifadhi makala zenye ukubwa wa 30MB (jumla ya makala zote). Utahitaji kuwa na makala nyingi na ndefu sana kuweza kufikia kiwango hicho kwa haraka. Ukifikia kuwa na makala za ukubwa huo unaweza kuanzisha akaunti mpya kwa jina jingine! Pia kuna kiwango cha ukubwa wa mafaili ambayo yanaweza kusomwa katika kipindi cha masaa 24 ambayo ni 15MB. Wasomaji wakisoma makala zenye ukubwa zaidi ya huo akaunti yako itasimama kwa muda (baadaye itaendelea kufanya kazi).

Muhimu: usipoitumia akaunti yako katika kipindi cha mwezi mzima itafungiwa kwa muda. Hivyo lazima uwe unaingia ndani ya akaunti hiyo (hata kama huna makala mpya za kuweka) mara kwa mara.

2. Box: http://www.box.net/

Huduma ya Box inakuwa nafasi kubwa zaidi ya Ripway ya kuhifadhi makala au hadithi zako. Una nafasi ya ukubwa gigabaiti 1 (IGB) bure. Ukitaka nafasi zaidi itabidi ulipie. Huduma hii inakuwezesha kubandika kiungo cha makala au hadithi yako kwenye blogu yako kwa ajili ya wasomaji wako.

3. Freefilehosting: http://www.freefilehosting.org/

Freefilehosting wanakupa nafasi ya ukubwa wa 50MB na pia kiungo cha makala ulizohifadhi ili uweze kuweka kwenye blogu yako.

4. Gimehost: http://www.gimehost.com/

Huduma ya Gimehost, ingawa haijajengwa vizuri kama Ripway inaweza kuchukua makala zako utakazoandika maisha yako yote, Yaani hakuna ukubwa wa mafaili ambao ndio kikomo. Pia wasomaji wanaweza kusoma makala zako bila kuzuiwa pale watakapokuwa wamesoma makala za ukubwa fulani. Huduma hii inakupa kiungo ambacho utakiweka kwenye blogu yako.

Jinsi ya kuweka kiungo cha makala kwenye blogu yako:

Ukishachagua huduma unayotaka, ukapandisha makala, utapewa kiungo/anuani ya webu. Nakili kiungo/anuani hiyo kisha ingia ndani ya blogu yako.

Kama unataka kuwa na kona maalum ya makala zako kwenye ufito wa pembeni (sidebar) itabidi ujue jinsi ya kuweka kichwa cha habari cha kona za makala zako. Maelezo hayo hapo chini:

<h2 class=”sidebar-title”> HAPA WEKA KICHWA/JINA LA KONA YA MAKALA ZAKO</h2>

* Weka jina la makala yako katikati ya alama: > na < (kama ilivyo hapo juu).

Halafu jinsi ya kuweka makala zenyewe kwenye ufito wa pembeni (sidebar), yaani chini ya jina la kona yako ya makala. Utachukua anuani/kiungo ulichopata toka kwenye huduma ya kuhifadhi makala (nilizozielezea hapo juu) na kuweka katikati ya alama za kufungua na kufunga usemi kama ilivyo hapo chini:

<ul>

<li><a href=”HAPA UTAWEKA ANUANI/KIUNGO CHA MAKALA YAKO”>HAPA UTAWEKA KICHWA CHA MAKALA YAKO AMBACHO NDIO KITAONEKANA KWA WASOMAJI KWENYE BLOGU</a></li>

</ul>

Kwahiyo kila utakapokuwa unaweka makala itabidi utumie muundo huo hapo juu. Jambo la kuhakikisha ni kuwa makala zote lazima ziwe katikati ya alama <ul> na </ul>. Hizi ndio “code” za kufunga na kufungua kwahiyo mambo yote weka hapo katikati.

Mahali pa kuweka ndani ya blogu: itabidi uingie ndani ya blogu kwa kutumia neno lako la siri. Kisha nenda panaposema: “change setting”, halafu bonyeza kwenye “template.” Kisha ndani ya templeti tafuta sehemu ambayo utapenda kuweka kona ya makala zako. Templeti zinatofautiana na kila mtu ana upenzi wake wa eneo analotaka kuweka makala. Ila ni vyema ukaweka chini ya “code” zinazoweka kisehemu cha maelezo binafsi (profile). Popote chini ya hapo ni sawa.

Ukiwa na swali usisite kuniuliza: ughaibuni@yahoo.com au kumuuliza mwanablogu mwingine yeyote aliyebobea.