Archive for the ‘Jinsi ya kuhamia Wordpress’ Category

Jinsi ya kuhamia WordPress toka Blogger

February 15, 2006

Naandika mwongozo huu wa namna ya kuhama toka Blogger (http://blogger.com  au http://blogspot.com) kwenda WordPress (http://wordpress.com) maana wanablogu wengi wa Kiswahili hivi sasa wanatumia huduma za Blogger.

WordPress ni huduma ambayo imetengenezwa kwa mtindo wa programu huria.  Hii inamaanisha kuwa wanaojenga programu hii na kuiboresha ni watu waliotapakaa pembe nne za dunia ambao wanafanya kazi hii kijamaa.  Zaidi ya kuwa kibinafsi ninapenda programu huria kutokana na itikadi na falsafa zangu binafsi, WordPress inatupa wanablogu uwezo wa kufanya mambo kadhaa ambayo yamekuwa hayawezekani kupitia Blogger.  Zaidi ya hilo, toleo la Kiswahili la WordPress liko njiani.  Soma hapa.  Utakapoanza kutumia WordPress utaona mwenyewe tofauti kubwa iliyopo kati yake na Blogger.  Kwa mfano, mpangilio wao wahabari katika maudhui na kisanduku cha kutafuta habari ulizoandika vinasaidia wasomaji kuweza kupata habari zako kwa urahisi.  Kwa mfano, ukija kwenye blogu yangu mpya ukataka kutafuta habari nilizoandika kuhusu Nyerere, unakwenda kwenye kisanduku cha kusaka habari na kuandika, “Nyererere,” ukibonyeza utapata habari zote nilizowahi kuandika kuhusu Nyerere. Upangaji wa habari kimaudhui unafanya habari zisipotelee kwenye “nyaraka” au “kumbukumbu” bali ziwe zinapatikana kwa urahisi.  Ni rahisi pia kupata kiungo cha habari yoyote tofauti na kwenye Blogger. Ukitaka kupata kiungo cha habari unayosoma (labda unataka kuweka kiungo hicho kwenye habari unayoandika kwenye blogu yako), unabonyeza juu ya kichwa cha habari yenyewe.  Utapalekwa kwenye kiungo chake.  Utaona kuwa kutokana na kutokuwa na mfumo huu kwenye Blogger, mwanablogu anaweza kuwa anazungumzia habari niliyoandika badala ya kuweka kiungo cha habari yenyewe akaweka kiungo cha blogu nzima. Kwa mfano, kiungo hiki ni cha blogu nzima: http://jikomboe.com, wakati ambapo kiungo hiki kinakupeleka moja kwa moja kwenye habari: http://www.jikomboe.com/?p=1108

Ukianza kutumia WordPress utaona ubora wake.  Unaweza kuanzisha blogu ya majaribio ili kutazama ilivyo.  Ukishaanzisha utaona kuwa WordPress ina mfumo mzuri wa “trackback” na “ping” ambao ni aina ya mawasiliano kati ya blogu na blogu.  Mifumo hii miwili inakuwezesha kujua nani ameweka kiungo cha blogu yako au habari uliyoandika kwenye blogu yake.  Mawasiliano haya anatokea bila wewe kufanya chochote. Taarifa hizi zinaingia zenyewe kwenye kidirisha cha maoni.

Hapo chini nimeweka maelezo yatakayokusaidia kama utakata shauri la kuhamia WordPress.  Kumbuka kuwa wakati wa kuhamisha blogu yakomambo kadhaa yatabadilika.  Itabidi uweke viungo upya na pia itakuwa vigumu picha kuhamishika moja kwa moja.  Soma maelezo:

Nenda http://wordpress.com

Bonyeza panaposema: Get a WordPress Blog Now.

WordPress watakutumia nywila (neno la siri) utakalotumia kuingia kwenye blogu yako.  Ukishaingia ndani ya blogu yako, nenda kwenye kisehemu kilichoko juu ya ukurasa kinachoitwa “Users.” Bonyeza hapo ili ubadilishe nywila waliyokutumia na kuweka nywila unayoitaka (ambayo utaikumbuka).

Ukishabonyeza hapo panaposema “Users,” tazama upande wa chini kulia ambapo utakuta panaposema, “Update your password.” Ukishachagua nywila mpya, bonyeza chini kabisa pasemapo, “Update profile.”

Baada ya hapo kazi inayofuata ni kuhamisha blogu yako toka blogger hadi wordpress. Kazi hii ni rahisi sana.  Tazama pale juu pembeni ya “Users,” utakuta panaposema, “Import.” Bonyeza hapo.  Kisha andika jina na neno la siri unalotumia kuingia kwenye blogu yako ya blogspot.com.   Halafu bonyeza panaposema, “start.” Jina la blogu yako litajitokeza. Bonyeza juu ya jina la blogu yako.  Wordpress itahamisha kila kitu toka blogger hadi wordpress.  Subiri hadi utakapoona maneno “congratulations.”  Hapo tazama chini kabisa kisha bonyeza panaposema, “Reset this importer.” Utaulizwa kama unataka kufanya hivyo au la. Bonyeza panaposema ndio.

Ili uone matokeo ya kazi uliyofanya, tazama juu kabisa, pembeni mwa jina la blogu yako hii mpya utaona panasema, “view site.” Bonyeza hapo utapelekwa kwenye blogu yako mpya ikiwa nay ale uliyoandika ukiwa blogspot.com .

Kutakuwa na mabadiliko kadhaa: kwa mfano picha si rahisi zihamishwe, viuongo ulivyoweka itabidi uweke upya, n.k.

Jambo muhimu na la kukumbuka ni kuwa kuanzia sasa utakuwa unaweza kuhifadhia kazi zako kwenye makundi ya kimaudhui.  Makundi haya (jina lake kwenye wordpress ni “categories”) unaweza kuyaweka wakati unapoandika jambo.  Ukiwa kwenye ukurasa wa kuandika jambo, tazama upande wa kulia utaona kuna mlolongo wa vitu ambapo “categories” ni mojawapo. Bonyeza  hapo, patatokea kisanduku ambacho utaweza kuandika jina la maudhui ya jambo unalotaka kuandika. Inaweza kuwa: utamaduni, siasa, muziki, safari, soka, n.k. Wewe utaamua.

Njia nyingine ya kuweka maudhui ni kwenda kwenye kisehemu cha “manage” kisha bonyeza kwenye kisehemu cha “categories,” halafu weka maudhui kwenye kisanduku cha “Add new category.”

Kumbuka kila unapoandika jambo lazima uweke alama ya vema kuonyesha ni katika maudhui gani au kundi gani unataka habari hiyo iwe.  Kama utaweka maudhui wakati unaandika habari na sio kupitia “manage” kisha “categories” (maelezo yake yako hapo juu) basi hutakuwa na haja ya kuweka alama ya vema maana alama hiyo itajiweka yenyewe.

Advertisements