Archive for the ‘Jinsi ya kuanza kublogu’ Category

Jinsi ya kuanza kublogu

April 7, 2006

Iwapo huna blogu na unataka kuanza, huduma ambayo inaweza kuwa rahisi sana kwako ni huduma ya Blogger. Huduma hii ni ya bure na ndio huduma maarufu sana kwa wanablogu wa Tanzania. Hatua za kufuata ni chache sana na rahisi kueleweka. Huduma yenyewe ya Blogger, ambayo mimi nilikuwa naitumia hapo awali, pengine ndio rahisi zaidi ya huduma nyingine kwa mtu ambaye ndio anaanza kublogu. Kumbuka kuwa ukianza kublogu kwa kutumia huduma moja, ukafika wakati ukataka kutumia huduma nyingine, unaweza kuhamisha blogu yako hiyo toka huduma ya zamani kwenda huduma mpya. Mimi, kwa mfano, nilikuwa natumia huduma ya blogger. Lakini sasa natumia huduma ya WordPress. Nimeweza kuhamisha blogu yangu nzima nzima bila matatizo.

Kwahiyo kitu cha kwanza cha kufanya ni kwenda kwenye tovuti ya Blogger kwa kubonyeza hapa. Ukifika pale kwenye tovuti yao, tazama upande wa chini kulia kuna alama ya mshale wa rangi ya machungwa unaosema: Create your blog now. Bonyeza juu ya mshale hu. Utapelekwa hatua kwa hatua toka mwanzo hadi mwisho ambapo kwa dakika chache tu utakuwa na blogu yako mwenyewe.

Ukiwa una mambo unayohitaji msaada, tazama ndani ya blogu hii (upande wa kulia kwenye "categories") ambapo utaona maelezo ya jinsi ya kuweka picha, viungo, jinsi ya kutangaza blogu yako, n.k. Au niandikie, au mwandikie mwanablogu yeyote wa Kiswahili maana tuna utamaduni wa kusaidiana kama ndugu. Usidhani kuwa utakuwa unatusumbua. Tunablogu na tunapenda nawe ujiunge na kijiji chetu uanze kublogu. Karibu!

Advertisements