Archive for June, 2006

Huduma muhimu za kutunza muda (muhimu sana kwa Afrika)

June 11, 2006

Moja ya huduma zinazonisaidia kutunza muda ni Bloglines. Huduma hii inachofanya ni kukusanya habari toka kwenye blogu au tovuti unazozipenda na kuzileta kwenye ukurasa mmoja. Kawaida ukitaka kusoma blogu upendazo unachofanya ni kuzitembelea (kwa kuandika anuani zake au kwa kupitia viungo katika blogu nyingine). Unapotembelea blogu hizo kuna wakati unakuta blogu ulizotembelea hazina habari au mambo mapya. Kitendo cha kutembelea blogu kumi ukakuta hakuna jambo jipya ni upotezaji wa muda. Ukitumia huduma ya Bloglines, huduma hii itakuwa inakuletea kwenye akaunti yako mambo mapya yaliyoandikwa kwenye blogu upendazo. Kwahiyo badala ya kutembelea blogu 10, moja baada ya nyingine, unatembelea ukurasa mmoja tu (yaani akaunti yako ndani ya bloglines) ambapo unaweza kusoma mambo yote mapya yaliyoandikwa kwenye blogu unazotaka.

Nizungumzia huduma ya Co.mments kabla ya kusema kwanini huduma au zana hizi ni muhimu kwa Afrika. Huduma ya Co.mments ni poa sana. Huduma hii inachofanya ni kukupa taarifa mpya toka sehemu ulizoacha maoni. Iwapo umetembelea blogu ya Jikomboe, ukaacha maoni. Wakati huo huo ukawa na hamu ya kujua wasomaji au wanablogu wengine watasema nini juu ya maoni uliyotoa, kawaida utakachofanya ni kurudi kila mara pale ulipoacha maoni ili kusoma maoni ya wengine na pengine kuendeleza mjadala. Huduma ya Co.mments inakusanya maoni yote mapya toka katika mijadala unayoshiriki na kukuletea katika akaunti yako.

Tuje kwa Afrika. Kwakuwa watumiaji wengi wa Intaneti Afrika wanatumia huduma za kulipia suala la muda ni muhimu sana. Ukienda mgahawa wa Intaneti, ukatembelea blogu 15, ukakuta zote hazina jambo jipya, hapo unakuwa umepoteza muda na fedha zako. Ukiwa kuna mjadala unaufuatilia katika kisehemu cha maoni kwenye blogu 9, kwa mfano, ukitembelea blogu hizo moja baada ya nyingine kutazama kama kuna maoni mapya, ukakuta blogu 2 tu ndio zina maoni mapya, hapo utakuwa umepoteza muda na fedha zako.

Tena, unajua kuwa kutokana na kiwango cha teknolojia ya Intaneti Afrika, kuna migahawa ambayo kasi ya mtandao wa Intaneti ni ndogo sana. Ina maana kuwa ukitembelea blogu 15 unaweza ukatumia saa nzima (hasa blogu zenyewe zikiwa zina picha, video au rangi rangi nyingi). Huduma za Bloglines na Co.mments zinakusaidia kwa kukusanya habari mpya na maoni mapya toka kwenye blogu idadi yoyote unayotaka (hata 1000) na kukuletea kwenye ukurasa mmoja. Kama unasoma blogu 25 kila unapoingia mtandaoni, badala ya kutembelea blogu 25 moja baada ya nyingine (na kupoteza muda wa kusubiri blogu itokee [kutokana na kasi ndogo ya mtandao] na baadaye kukuta kuwa hakuna jipya) unatembelea tovuti moja tu na kukuta mambo yote mapya toka kwenye blogu hizo 25. Kwa maneno mengine, unatembelea blogu moja inayokuwezesha kutembelea blogu 25 “bila kuzitembelea.” Hivi ndiyo ilivyo pia kwa maoni. Badala ya kutembelea blogu 8 ambazo zina mijadala unayofuatilia, unatembelea ukurasa mmoja tu wa Co.mments ambapo maoni yote mapya toka kwenye blogu hizo 8 yatakuwa yakikusubiri.

Zana/huduma hizi ni utaona faida yake iwapo wewe unatumia huduma za Intaneti za kulipia na zenye kasi ndogo, na pia kama wewe ni msomaji wa blogu na tovuti nyingi kama mimi. Na pia kama unapenda kufuatilia mijadala fulani fulani inayoendeshwa katika sehemu za maoni ndani ya blogu. Kama wewe ni mtu ambaye umebanwa na shughuli hivyo kila dakika kwako ni muhimu, unaweza kutumia huduma hizi kutunza muda.

Bonyeza hapa ukitaka kujiandikisha kutumia huduma ya Co.mments. Kwa huduma ya Bloglines, bonyeza hapa.

Advertisements