Archive for April, 2006

Jinsi ya kuwatumia wasomaji habari unazoandika

April 16, 2006

Yapo mambo kadhaa ambayo mwenye blogu anaweza kufanya ili kusaidia wasomaji kwa kurahisisha upatikanaji wa habari unazoandika. Kati ya mambo hayo ni huduma inayowezesha wasomaji kutumiwa mambo unayoandika kwa barua pepe. Msomaji anachotakiwa kufanya ni kuweka anuani yake kwenye fomu utakayoweka kwenye blogu yako kisha atatumiwa habari mpya kila unapoandika. Huduma nitakazokupa ni za bure (ingawa zipo pia za kulipia). Kama ungependa kuwapa wasomaji wako huduma hii, unaweza kutumia huduma kati ya hizi nitakazoorodhesha hapo chini. Ukiwa na tatizo ya jinsi ya kutumia huduma hizo au kuziweka kwenye blogu yako unaweza kuniandikia: ughaibuni@yahoo.com (HAKIKISHA KICHWA CHA WARAKA WAKO KINASEMA: MWONGOZO WA BLOGU)(LA SIVYO BARUA YAKO INAWEZA IKACHUKUA MUDA MREFU KUSOMWA).

Huduma ni hizi:

1. FEEDBLITZ: http://www.feedblitz.com/

2. SQUEET: http://www.squeet.com/

3. YUTTER: http://www.yutter.com/

4. AWEBER: http://www.buniek.com/

5. ZOOKODA: http://www.zookoda.com/

Advertisements

Huduma za kuhifadhi makala ndefu na Jinsi ya kuweka makala bloguni

April 15, 2006

Iwapo unaandika makala ndefu (waandishi wa habari hupenda kuita makala ndefu “mikeka”) au labda wewe ni mwanasafu na unapenda kuweka makala zako kwenye blogu yako, zipo huduma kadhaa ambazo unaweza kutumia ili kuhifadhi makala hizo. Kisha utanakili anuani ya makala zako toka kwenye huduma uliyotumia na kubandika kwenye blogu yako. Msomaji akibonyeza ulipoweka kiungo cha makala hiyo ataweza kuisoma. Huduma hizi ni za bure (zipo pia za kulipia ila nadhani hakuna sababu za msingi za kuacha kutumia huduma hizi za bure).

Huduma zenyewe:

1. Ripway: http://www.ripway.com

Huduma hii inatumiwa na wanablogu wengi wa Kiswahili. Huduma hii ni nzuri ingawa ina kiwango cha ukubwa wa mafaili ambayo unaweza ukahifadhi hapo. Unaweza kuhifadhi makala zenye ukubwa wa 30MB (jumla ya makala zote). Utahitaji kuwa na makala nyingi na ndefu sana kuweza kufikia kiwango hicho kwa haraka. Ukifikia kuwa na makala za ukubwa huo unaweza kuanzisha akaunti mpya kwa jina jingine! Pia kuna kiwango cha ukubwa wa mafaili ambayo yanaweza kusomwa katika kipindi cha masaa 24 ambayo ni 15MB. Wasomaji wakisoma makala zenye ukubwa zaidi ya huo akaunti yako itasimama kwa muda (baadaye itaendelea kufanya kazi).

Muhimu: usipoitumia akaunti yako katika kipindi cha mwezi mzima itafungiwa kwa muda. Hivyo lazima uwe unaingia ndani ya akaunti hiyo (hata kama huna makala mpya za kuweka) mara kwa mara.

2. Box: http://www.box.net/

Huduma ya Box inakuwa nafasi kubwa zaidi ya Ripway ya kuhifadhi makala au hadithi zako. Una nafasi ya ukubwa gigabaiti 1 (IGB) bure. Ukitaka nafasi zaidi itabidi ulipie. Huduma hii inakuwezesha kubandika kiungo cha makala au hadithi yako kwenye blogu yako kwa ajili ya wasomaji wako.

3. Freefilehosting: http://www.freefilehosting.org/

Freefilehosting wanakupa nafasi ya ukubwa wa 50MB na pia kiungo cha makala ulizohifadhi ili uweze kuweka kwenye blogu yako.

4. Gimehost: http://www.gimehost.com/

Huduma ya Gimehost, ingawa haijajengwa vizuri kama Ripway inaweza kuchukua makala zako utakazoandika maisha yako yote, Yaani hakuna ukubwa wa mafaili ambao ndio kikomo. Pia wasomaji wanaweza kusoma makala zako bila kuzuiwa pale watakapokuwa wamesoma makala za ukubwa fulani. Huduma hii inakupa kiungo ambacho utakiweka kwenye blogu yako.

Jinsi ya kuweka kiungo cha makala kwenye blogu yako:

Ukishachagua huduma unayotaka, ukapandisha makala, utapewa kiungo/anuani ya webu. Nakili kiungo/anuani hiyo kisha ingia ndani ya blogu yako.

Kama unataka kuwa na kona maalum ya makala zako kwenye ufito wa pembeni (sidebar) itabidi ujue jinsi ya kuweka kichwa cha habari cha kona za makala zako. Maelezo hayo hapo chini:

<h2 class=”sidebar-title”> HAPA WEKA KICHWA/JINA LA KONA YA MAKALA ZAKO</h2>

* Weka jina la makala yako katikati ya alama: > na < (kama ilivyo hapo juu).

Halafu jinsi ya kuweka makala zenyewe kwenye ufito wa pembeni (sidebar), yaani chini ya jina la kona yako ya makala. Utachukua anuani/kiungo ulichopata toka kwenye huduma ya kuhifadhi makala (nilizozielezea hapo juu) na kuweka katikati ya alama za kufungua na kufunga usemi kama ilivyo hapo chini:

<ul>

<li><a href=”HAPA UTAWEKA ANUANI/KIUNGO CHA MAKALA YAKO”>HAPA UTAWEKA KICHWA CHA MAKALA YAKO AMBACHO NDIO KITAONEKANA KWA WASOMAJI KWENYE BLOGU</a></li>

</ul>

Kwahiyo kila utakapokuwa unaweka makala itabidi utumie muundo huo hapo juu. Jambo la kuhakikisha ni kuwa makala zote lazima ziwe katikati ya alama <ul> na </ul>. Hizi ndio “code” za kufunga na kufungua kwahiyo mambo yote weka hapo katikati.

Mahali pa kuweka ndani ya blogu: itabidi uingie ndani ya blogu kwa kutumia neno lako la siri. Kisha nenda panaposema: “change setting”, halafu bonyeza kwenye “template.” Kisha ndani ya templeti tafuta sehemu ambayo utapenda kuweka kona ya makala zako. Templeti zinatofautiana na kila mtu ana upenzi wake wa eneo analotaka kuweka makala. Ila ni vyema ukaweka chini ya “code” zinazoweka kisehemu cha maelezo binafsi (profile). Popote chini ya hapo ni sawa.

Ukiwa na swali usisite kuniuliza: ughaibuni@yahoo.com au kumuuliza mwanablogu mwingine yeyote aliyebobea.

Jinsi ya kuanza kublogu

April 7, 2006

Iwapo huna blogu na unataka kuanza, huduma ambayo inaweza kuwa rahisi sana kwako ni huduma ya Blogger. Huduma hii ni ya bure na ndio huduma maarufu sana kwa wanablogu wa Tanzania. Hatua za kufuata ni chache sana na rahisi kueleweka. Huduma yenyewe ya Blogger, ambayo mimi nilikuwa naitumia hapo awali, pengine ndio rahisi zaidi ya huduma nyingine kwa mtu ambaye ndio anaanza kublogu. Kumbuka kuwa ukianza kublogu kwa kutumia huduma moja, ukafika wakati ukataka kutumia huduma nyingine, unaweza kuhamisha blogu yako hiyo toka huduma ya zamani kwenda huduma mpya. Mimi, kwa mfano, nilikuwa natumia huduma ya blogger. Lakini sasa natumia huduma ya WordPress. Nimeweza kuhamisha blogu yangu nzima nzima bila matatizo.

Kwahiyo kitu cha kwanza cha kufanya ni kwenda kwenye tovuti ya Blogger kwa kubonyeza hapa. Ukifika pale kwenye tovuti yao, tazama upande wa chini kulia kuna alama ya mshale wa rangi ya machungwa unaosema: Create your blog now. Bonyeza juu ya mshale hu. Utapelekwa hatua kwa hatua toka mwanzo hadi mwisho ambapo kwa dakika chache tu utakuwa na blogu yako mwenyewe.

Ukiwa una mambo unayohitaji msaada, tazama ndani ya blogu hii (upande wa kulia kwenye "categories") ambapo utaona maelezo ya jinsi ya kuweka picha, viungo, jinsi ya kutangaza blogu yako, n.k. Au niandikie, au mwandikie mwanablogu yeyote wa Kiswahili maana tuna utamaduni wa kusaidiana kama ndugu. Usidhani kuwa utakuwa unatusumbua. Tunablogu na tunapenda nawe ujiunge na kijiji chetu uanze kublogu. Karibu!

Jinsi ya kublogu kwa simu za mkono

April 7, 2006

Badala ya kublogu kwa kutumia tarakilishi (kompyuta) unaweza kublogu kwa kutumia simu ya mkono. Zipo huduma kadhaa, za bure na pia za kulipia, ambazo zinakuwezesha kutumia simu ya mkono kublogu. Huduma maarufu ya kublogu ya Blogger inayo huduma ya kublogu kwa simu (Audioblogger). Bonyeza hapa upate maelezo ya jinsi ya kutumia huduma hiyo. Kumbuka: lazima ujiandikishe kwanza kwenye huduma ya Blogger ili uweze kutumia huduma ya Audioblogger. Jinsi ya kujiandikisha kwenye Blogger, bonyeza hapa.

Huduma nyingine ni Phoneblogz. Huduma hii inakuwezesha kutuma ujumbe wa sauti, kwa kutumia simu, kwenye blogu yako. Bonyeza hapa uione huduma hiyo. Kuna huduma iitwayo Gabcast. Huduma hii nayo inakuwezesha kutuma ujumbe wa sauti kwenye blogu yako. Lakini pia unaweza kuanzisha blogu ya sauti kwa kutumia huduma yao. Gabcast wana huduma ya bure na nyingine ya kulipia. Bonyeza hapa uende kwenye tovuti yao.

Huduma nyingine iitwayo Phlogger inakuwezesha kublogu kwa kutumia simu ya mkono ila badala ya kutuma ujumbe kwa sauti kama huduma nilizotaja hapo juu, huduma hii inakuwezesha kutuma ujumbe wa maandishi. Bonyeza hapa uitazame.