January 15, 2018

Earn free bitcoin

Jinsi ya Kuweka Video Kwenye Blogger/Blogspot

August 26, 2007

Baada ya huduma ya kublogu ya Blogger kununuliwa na Google, nilidhani kuwa wangeboresha huduma zao haraka. Naona hawana haraka. Bado zana kama WordPress zinamwezesha mtumiaji kufanya mambo mengi zaidi na kwa urahisi.

Lakini wiki hii Blogger wametoa habari njema, sasa unaweza kupandisha video kama jinsi ilivyo rahisi kupandisha picha. Yeeeee! Kwa watumiaji wa Blogger, kazi kwenu. Tuleteeni video zenu. Bonyeza hapa usome jinsi ya kutumia huduma hiyo.

RSS Ni Kitu Gani?

May 13, 2007

Huenda umewahi kusikia kuhusu RSS lakini bado hujaelewa vizuri kuwa huyu ni mdudu gani. RSS ni teknolojia muhimu sana kwa wasomaji wa habari mtandaoni, wanablogu, wenye tovuti, n.k.  Jamaa wa BloggingPro wametengeneza video nzuri mno inayoeleza kwa kifupi na lugha rahisi maana ya RSS na jinsi utakavyoweza kuitumia. Bonyeza hapa uitazame na kujifunza.

Snap: Huduma ya Kuweka Picha Kwenye Viungo

December 31, 2006

Iwapo unapenda wasomaji wako kuona picha ndogo ya tovuti au blogu ambayo umeweka kiungo chake kwenye habari unayoandika, unaweza kutumia huduma ya Snap. Huduma hii inawezesha wasomaji kuweza kuiona tovuti au blogu kabla ya kubonyeza na kuitembelea.

Nimeijaribu huduma hii kwenye blogu yangu ya Jikomboe na imefanya kazi bila matatizo yoyote. Unachotakiwa kufanya ni kufuata maelekezo yaliyoko hapa. Au kama wewe unatumia huduma ya Blogger unaweza kupata maelezo hapa na kwa watumiaji wa WordPress, maelekezo haya hapa.  

Zana ya kutengeneza Blogu au Tovuti Yako

December 26, 2006

Mwezi wa nane mwaka huu niliandika kuhusu huduma ya Wetpaint ambayo inakuwezesha kujenga blogu, wiki, au tovuti yako mwenyewe bila kuwa na haja ya kujua lugha ya kujenga tovuti (HTML au nyinginezo) na pia bila kutakiwa kushusha programu yoyote kwenye kompyuta yako. Huduma kama hizi ni muhimu sana kwa watu walioko katika nchi za Kusini ambapo wengi wanatumia kompyuta ambazo sio zao (kwenye migahawa) hivyo inakuwa vigumu kushusha programu kwenye kompyuta hizo. Pia inakuwa vigumu kutumia muda mrefu kwenye kompyuta kujifunza mambo kama ujenzi wa tovuti toka A hadi Z. Bonyeza hapa usome niliyoandika kuhusu Wetpaint na huduma nyingine.

Sasa kampuni ya incuBeta ina huduma inayofanana kiasi na Wetpaint ambayo inaitwa Synthasite. Huduma hii bado iko kwenye matengenezo ila unaweza kuwapa anuani yako ili wakutaarifu itakapokuwa tayari. Bonyeza hapa.

Scoopt: Huduma Poa Kwa Wanablogu wa Picha na Wapiga Picha

December 26, 2006

Iwapo wewe ni mwanablogu wa picha au mpiga picha na ungependa uwe unauza picha zako, kuna huduma inaitwa Scoopt. Huduma hii inachofanya ni kutafuta vyombo vya habari ambavyo vitanunua picha yako kisha mnagawa mapato nusu kwa nusu. Wewe asilimia 50 na wao 50. Mchezo umekwisha. Ila picha zenyewe lazima ziwe zinauzika na sio picha za familia yako, mbwa wako, majirani wako, n.k. Bonyeza hapa utembelee tovuti ya Scoopt. Ukitaka kujua aina ya picha ambazo wanazipenda, bonyeza hapa.

Iwapo unatumia huduma ya Flickr kuhifadhi picha zako, na ungependa jamaa wa Scoopt wazipate picha zako, unashauriwa kutumia neno “scoopt” kama neno la kuashiria maudhui ya picha yako (kwa kiingereza “tag”).

Ndesanjo, Hivi Blogu ni nini?

September 1, 2006

Watu wengi tunajiuliza blogu ni kitu gani? Tunatembelea blogu, tunazisoma, tunashawishika kutaka kuanzisha zetu, ila bado tunakuwa tunajiuliza, “blogu ni nini?” Soma makala nilizoandikwa kwa ajili ya gazeti la Mwananchi kujaribu kutoa jibu la swali hili. Makala hizi ziko katika sehemu tatu. Bonyeza hapa.

Pia kuna makala fupi katika Wikipedia ya Kiswahili inayojibu swali: blogu ni nini? Bonyeza hapa uisome.

Zana ya kutengeneza blogu au tovuti yako

August 12, 2006

Kuna zana mpya ambayo itawafaa sana watu wenye nia ya kuwa na tovuti, blogu, au wiki zao wenyewe lakini hawana ujuzi wa utalaamu unaotumika kutengeneza tovuti, blogu, au wiki.  Zana hii inaitwa Wetpaint. Kwa dakika chache na bila ujuzi wowote zaidi ya ujuzi wa kutumia tarakilishi, unaweza kuwa na blogu au tovuti yako mwenyewe. Bonyeza hapa ujionee mwenyewe. Majuzi niliandika kuhusu zana hiyo na nyingine zinazofanana katika blogu yangu, bonyeza hapa na hapa ili usome niliyoandika.

Jiandikishe kwenye ukurasa huria wa Global Voices

July 9, 2006

Unapofungua blogu yako usisahau kuiorodhesha katika ukurasa huria (wiki) wa mradi wa Global Voices. Iwapo wewe ni mwanablogu toka Kenya, bonyeza hapa kisha ongeza blogu yako katika orodha. Iwapo wewe umetoka Tanzania bonyeza hapa.

Ukifika katika ukurasa huo, tazama sehemu ambayo blogu yako inapaswa kuwepo (ipo shemeu ya blogu za Kiswahili, blogu za lugha zaidi ya moja, blogu ya picha, n.k.) kisha bonyeza sehemu isemayo “edit” iliyo juu upande wa kulia wa sehemu unayotaka kuorodhesha blogu yako.

Huduma muhimu za kutunza muda (muhimu sana kwa Afrika)

June 11, 2006

Moja ya huduma zinazonisaidia kutunza muda ni Bloglines. Huduma hii inachofanya ni kukusanya habari toka kwenye blogu au tovuti unazozipenda na kuzileta kwenye ukurasa mmoja. Kawaida ukitaka kusoma blogu upendazo unachofanya ni kuzitembelea (kwa kuandika anuani zake au kwa kupitia viungo katika blogu nyingine). Unapotembelea blogu hizo kuna wakati unakuta blogu ulizotembelea hazina habari au mambo mapya. Kitendo cha kutembelea blogu kumi ukakuta hakuna jambo jipya ni upotezaji wa muda. Ukitumia huduma ya Bloglines, huduma hii itakuwa inakuletea kwenye akaunti yako mambo mapya yaliyoandikwa kwenye blogu upendazo. Kwahiyo badala ya kutembelea blogu 10, moja baada ya nyingine, unatembelea ukurasa mmoja tu (yaani akaunti yako ndani ya bloglines) ambapo unaweza kusoma mambo yote mapya yaliyoandikwa kwenye blogu unazotaka.

Nizungumzia huduma ya Co.mments kabla ya kusema kwanini huduma au zana hizi ni muhimu kwa Afrika. Huduma ya Co.mments ni poa sana. Huduma hii inachofanya ni kukupa taarifa mpya toka sehemu ulizoacha maoni. Iwapo umetembelea blogu ya Jikomboe, ukaacha maoni. Wakati huo huo ukawa na hamu ya kujua wasomaji au wanablogu wengine watasema nini juu ya maoni uliyotoa, kawaida utakachofanya ni kurudi kila mara pale ulipoacha maoni ili kusoma maoni ya wengine na pengine kuendeleza mjadala. Huduma ya Co.mments inakusanya maoni yote mapya toka katika mijadala unayoshiriki na kukuletea katika akaunti yako.

Tuje kwa Afrika. Kwakuwa watumiaji wengi wa Intaneti Afrika wanatumia huduma za kulipia suala la muda ni muhimu sana. Ukienda mgahawa wa Intaneti, ukatembelea blogu 15, ukakuta zote hazina jambo jipya, hapo unakuwa umepoteza muda na fedha zako. Ukiwa kuna mjadala unaufuatilia katika kisehemu cha maoni kwenye blogu 9, kwa mfano, ukitembelea blogu hizo moja baada ya nyingine kutazama kama kuna maoni mapya, ukakuta blogu 2 tu ndio zina maoni mapya, hapo utakuwa umepoteza muda na fedha zako.

Tena, unajua kuwa kutokana na kiwango cha teknolojia ya Intaneti Afrika, kuna migahawa ambayo kasi ya mtandao wa Intaneti ni ndogo sana. Ina maana kuwa ukitembelea blogu 15 unaweza ukatumia saa nzima (hasa blogu zenyewe zikiwa zina picha, video au rangi rangi nyingi). Huduma za Bloglines na Co.mments zinakusaidia kwa kukusanya habari mpya na maoni mapya toka kwenye blogu idadi yoyote unayotaka (hata 1000) na kukuletea kwenye ukurasa mmoja. Kama unasoma blogu 25 kila unapoingia mtandaoni, badala ya kutembelea blogu 25 moja baada ya nyingine (na kupoteza muda wa kusubiri blogu itokee [kutokana na kasi ndogo ya mtandao] na baadaye kukuta kuwa hakuna jipya) unatembelea tovuti moja tu na kukuta mambo yote mapya toka kwenye blogu hizo 25. Kwa maneno mengine, unatembelea blogu moja inayokuwezesha kutembelea blogu 25 “bila kuzitembelea.” Hivi ndiyo ilivyo pia kwa maoni. Badala ya kutembelea blogu 8 ambazo zina mijadala unayofuatilia, unatembelea ukurasa mmoja tu wa Co.mments ambapo maoni yote mapya toka kwenye blogu hizo 8 yatakuwa yakikusubiri.

Zana/huduma hizi ni utaona faida yake iwapo wewe unatumia huduma za Intaneti za kulipia na zenye kasi ndogo, na pia kama wewe ni msomaji wa blogu na tovuti nyingi kama mimi. Na pia kama unapenda kufuatilia mijadala fulani fulani inayoendeshwa katika sehemu za maoni ndani ya blogu. Kama wewe ni mtu ambaye umebanwa na shughuli hivyo kila dakika kwako ni muhimu, unaweza kutumia huduma hizi kutunza muda.

Bonyeza hapa ukitaka kujiandikisha kutumia huduma ya Co.mments. Kwa huduma ya Bloglines, bonyeza hapa.